BAKWATA, MAREKANI WALAANI VURUGU ZANZIBAR

Na Waandishi Wetu
BALOZI wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhardt, amesema kuwa nchi yake imesikitishwa na machafuko ya siku mbili yaliyosababisha uvunjifu wa amani hapa Zanzibar.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Balozi Lenhardt alisema fujo zilizotokea ni za kusikitisha na kutaka hatua za haraka zichukuliwe katika kurejesha amani visiwani Zanzibar.

Balozi huyo alitaka viongozi wa kisiasa kushiriki kikamilifu katika kuirejesha amani, ambapo alisema machafuko ya siku mbili yameharibu sifa nzuri ya amani iliyopo Zanzibar, hasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.


Balozi Lenhardt alisema amani ni suala muhimu sana kwa visiwa vya Zanzibar kwani kwa kiasi kikubwa uchumi wa visiwa hivyo umekuwa ukitegemea sekta ya utalii ambayo huimarika zaidi panapotawala amani na utulivu.

Katika hatua nyengine Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limelaani vurugu na machafuko yaliyotokea Zanzibar, ambayo yamesababisha kuchomwa makanisa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, msemaji wa vijana wa Baraza hilo Said Mwaipopo, alisema kuwa waislamu si watu wa vurugu na kwamba watu wamefanya kwa kutumia kusingizio cha dini.

Alifahamisha kuwa hakuna sehemu yoyote katika kitabu kituku cha qur-ani ambacho kinahamasisha vurugu dhidi ya dini nyengine na kwamba vurugu hizo zimefanywa na watu kwa kisingizio cha dini kupitia jumuiya ya UAMSHO.

Akizungumzia madai ya kikundi cha UAMSHO juu ya kupinga Muungano, Mwaipopo alisema kama kunahitajika kutoa maoni juu ya Muungano isubiriwe tume iliyoundwa kwani ndiyo yenye kazi ya kukusanya maoni juu ya katiba mpya.

“Kama kuna lolote wanalolipinga dhidi ya Muungano, wawakataze wajumbe kuingia kwenye tume hiyo pia wabunge wasishiriki, lakini hakuna maoni yatakayopokelewa kwa kufanya vurugu na kuharibu mali za wasiohusika”, alisema.

Nacho Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA), kimevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinarejesha hali ya amani na utulivu pamoja na kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya waliohusika na matukio ya vurugu.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar, Hamad Yussuf alisema vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua jitihada za kudhibiti fujo zinazofanywa na vijana ambao wana lengo la kutaka kuvunja amani na utulivu uliopo.

Aidha aliwataka wananchi kushirikiana na vyombo hivyo ili wale wote waliohusika na ufanyaji fujo huo uliosababisha haarsa kubwa wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Hamad, alisema Muungano hauwezi kupingwa kwa vurugu na kuwataka wananchi wajipange kwa hoja zitakazoweza kuandikwa katiba ambayo itaondoshwa mizwengwe iliyopo katika Muungano.

Alivitaka vyama vya siasa kuacha kuandaa makundi ya vijana ambao mwisho wake wanakosa kuwapatia kazi, hali inayowafanya hukosa shughuli za kufanya na hatimaye kuwa na vikundi vya kihalifu.

Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Zanzibar kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kutokea kwa fujo zilizopelekea uchomwaji moto gari, nyumba za ibada na nyumba za wananchi.

Nacho Chama cha CUF, kimesema kuwa machafuko yaliyotokea yamesababishwa na wachochezi wasiopenda kuona serikali ya Umoja wa Kitaifa inanawiri visiwani Zanzibar.

Akitoa taarifa ya Chama hicho Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu, Habari, Uenenzi na Mawasiliano ya Umma, Salum Bimani alisema CUF haiwezi kukaa kimya kuona hali tete ya kuchezewa kwa amani ikitokea.

“Chama cha CUF, kinatoa wito kwa wananchi wote kuwa watulivu, wavumilivu, na kuitumia fursa ya kutoa mawazo yao bila ya jazba, pamoja na kutowanyima wengine nafasi ya kuwasilisha mitazamo yao”, alisema Bimani katika taarifa hiyo.

Alibainisha kuwa vitendo vya watu wachache kuchoma makanisa na kuharibu mali za watu ni vya uvunjifu wa sheria na kinyume na utamaduni wa Kizanzibari na kutaka uchunguzi wa kina ufanyike na waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria, bila uonevu wala upendeleo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.