CHADEMA, SHIBUDA SASA JINO KWA JINO

MBUNGE wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), amemshukia Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha) wa chama hicho, John Heche akimta amwombe radhi ndani ya siku tatu, vinginevyo atamshtaki kwa umma.

Shibuda alitoa kauli hiyo jana akitaka Heche atekeleze hilo ndani ya siku tatu, alipozungumza na vyombo vya habari kuhusu kauli zilizotolewa na Bavicha kuwa mbunge huyo ataondolewa ubunge.

Mbali na kumnyooshea kidole Heche, Shibuda alikwenda mbali zaidi na kumtaka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa kuwa meneja wake wa kampeni katika harakati zake za kuingia Ikulu mwaka 2015 akisema, Dk Slaa atasaidiana na Rais Jakaya Kikwete katika kazi hiyo.

 “Inaonekana Heche ana mtindio wa ubongo na wala si mzima wa akili yule, maana habari ya kutangaza kuwania urais ni haki ya kila mmoja. Hata nilipokuwa CCM mara kadhaa nilitangaza, lakini UVCCM haikutoa tamko, wala hakuna mtu wa usalama aliyekuja kunigongea. Iweje leo huku?” alisema akihoji na kuongeza:

“Kule CCM nilikimbia dhuluma na huku siwezi kukubali dhuluma, ndiyo maana nimekuwa mkimya kwa muda mrefu nikisoma mazingira. Lakini wakati wa kuzungumza umefika kwa kuwa ni haki yangu, huku nikitambua kuwa nchi inajengwa na wenye moyo na inaliwa na wenye meno.’’

Alisema kuwa kutangaza nia ya kugombea urais ni haki ya kila mmoja na kwamba, Katiba ya Tanzania inamruhusu kila mmoja kufanya hivyo, lakini kinachotokea kwa Bavicha ni uhuni na wendawazimu unaokwenda sanjari na ulimbukeni.

Akizungumza kwa jazba na kutumia misamiati mingi, Shibuda alisema kuwa kinachofanywa na Heche ni msumari wa jeneza la kuua demokrasia na kutaka kumzika yeye kisiasa, akisema kuwa hatanyamaza hadi kifo chake.

“Heche anatengeneza jeneza la kunizika kisiasa, siwezi kunyamaza na viongozi wa juu wanajua kwamba Shibuda siyo wa kunyamaza na hawezi kunipora uanachama wangu hata siku moja kwani nimesimama imara ndani ya Chadema,’’ aliongeza.

Mbunge huyo alimtaka Mwenyekiti wa Chadema Taifa kuitisha kikao mara moja na kujadili uwezo wa Heche na ikibidi wamfukuze mara moja ndani ya chama kwa kuwa anawagawa wananchi kwa ukabila na kwamba yupo kwa ajili ya masilahi ya wachache.

Kuhusu madai ya kutiliwa shaka ndani ya chama, alisema kuwa ni utaratibu wa kawaida kwa mwanasiasa mwenye mvuto kupambana na matatizo hayo, huku akisifu uwezo wa Mbowe akisema kuwa, amekuwa akiwatuliza wanachama wa Chadema kwa kuwa ameelewa msimamo wake (Shibuda) ni upi.

Akizungumzia nafasi yake ndani ya Chadema alisema hana shaka na uanachama wake na kwamba kinachomponza ni yeye (Shibuda) ni uwazi na ukweli, lakini hayupo katika kukisaliti chama.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*