CHADEMA:CCM NI YA MAFISADI

BARAZA Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limesema kuwa mabadiliko ya baraza la mawaziri yanayotarajiwa kufanyika wakati wowote si suluhu ya kupunguza au kumaliza ubadhirifu serikalini kwa madai kuwa ufisadi ni sehemu ya mfumo wa utawala wa CCM.
Aidha kuvunjwa kwa baraza la mawaziri kwa kuepuka ushauri wa wabunge na kutumia kauli ya Kamati Kuu ya CCM, ni matokeo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kuhofia nguvu ya umma.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari akielezea maazimio ya baraza hilo lililomaliza kikao chake juzi.
Mnyika alieleza kuwa mabadiliko hayo hayataleta mageuzi ya maana kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete bado atateua sehemu kubwa ya mawaziri waliopatikana kifisadi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
“Kauli ya CCM kuwa watawapeleka mahakamani mawaziri na watendaji wote waliohusika katika ubadhirifu ni siasa tupu, kwani ushahidi uko wazi kuwa mpaka sasa serikali hiihii chini ya chama hichohicho haijawapeleka mahakamani mawaziri waliopatikana na kashfa na kulazimika kujiuzulu mwaka 2008 na wameshindwa kuwafukuza kwenye chama.
“Zaidi ya hayo, kuna orodha ndefu ya mafisadi iliyotolewa hadharani mwaka 2007 na mafisadi wakuu hawajagushwa,” alisema.
Alieleza kuwa CCM iliitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu na kutoa tamko juu ya baraza la mawaziri baada ya kusikia kuwa Baraza Kuu la chama hicho linakutana na kuanza maandalizi ya kuunganisha nguvu ya umma kushinikiza mabadiliko ya kiutawala na mfumo.
“…ni wazi kuwa CCM na Rais Jakaya Kikwete wamekubali kufikia hatua hiyo wakihofia nguvu ya umma.
“Baraza Kuu limeazimia kuwataka Watanzania kutambua kuwa kwa muda mrefu sasa baraza la mawaziri limekuwa kielelezo kamili cha mfumo wa ubadhirifu, rushwa na ufisadi katika utawala wa nchi hii chini ya CCM,” alisema Mnyika.
Alisema chama hicho si cha msimu wala matukio na kwamba wanahitaji uwajibikaji mkubwa nchini na kuongeza kuwa operesheni za chama hicho nchi nzima hazitakwisha.
“Operesheni zetu ziko palepale, tunahitaji mabadiliko ya mfumo, kwani kuna uozo mkubwa kwenye safu za uongozi,” alisema Mnyika wataunganisha nguvu ya umma na kujenga chama katika operesheni hizo.
Hali ya uchumi
Mnyika alisema kuwa baraza hilo limebaini kuwa hali hiyo inasababishwa na uongozi dhaifu wa serikali ya CCM ambayo imeshindwa kudhibiti matumizi mabaya katika serikali na idara zake na kushindwa kuchochea uzalishaji wa chakula na nishati nchini.
Alisema kuwa baraza hilo limeuagiza uongozi wa taifa wa CHADEMA pamoja na wabunge kuwahimiza wananchi kuendelea kuishinikiza serikali kutimiza wajibu wake.
Pamoja na hilo, alisema baraza hilo limewataka wananchi kujiandaa kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi na utawala katika chaguzi zijazo, kwani kikwazo kikubwa cha maendeleo nchini ni CCM inayoendesha serikali kwa mfumo wa rushwa na ufisadi.
Mnyika aliongeza kuwa mabadiliko ya kweli nchini yatapatikana kwa kuiondoa CCM madarakani.
Mauaji ya wanachama
Baraza hilo limelaani mauaji ya wanachama wake huku jeshi la polisi likishindwa kuchukua hatua zozote za maana.
“Baraza Kuu limelaani mauaji ya Mwenyekiti wa Kata ya Usa River yaliyotokea Aprili 28 mwaka huu na pia limeeleza kusikitishwa na jeshi la polisi kwa kushindwa kuchukua hatua za maana dhidi ya watu waliohusika na mauaji ya wanachama wa CHADEMA ambayo yamekuwa yakitokea tangu uchaguzi mdogo wa Igunga,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, alisema baraza hilo limeuagiza uongozi wa chama hicho kuanzisha mchakato wa kulishtaki jeshi la polisi kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake.
Aidha pamoja na hayo, alisema baraza hilo limeagiza chama kusukuma hoja ya kuwapo kwa uchunguzi huru dhidi ya matendo ya kidhalimu yanayofanywa na Jeshi la Polisi na kutolea mfano Arusha, Mwanza, Ruvuma Mbeya na Mtwara (Tandahimba).
Uchaguzi ndani ya chama
Mnyika alisema kikao hicho kimepanga uchaguzi ndani ya chama hicho kufanyika kuanzia Juni mwaka huu kwa ngazi ya msingi na kukamilika Oktoba mwakani kwa ngazi ya taifa.
alisema katika kudhibiti rushwa katika uchaguzi huo, baraza kuu limeiagiza Kamati Kuu kuandaa mwongozo wa kudhibiti hali hiyo, ili kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa uadilifu na maadili.
Masuala ya kijamii
Aidha alisema baraza hilo limeitaka serikali ya CCM kutekeleza tamko la chama hicho kutatua migogoro ya makundi ya kijamii kama wanafunzi, wafanyakazi, wakulima hasa katika masuala ya ardhi na maslahi ya wafanyakazi.
Alisema kuwa mpaka sasa serikali bado haijapandisha mishahara ya wafanyakazi na kusema kuwa hali hiyo ndiyo inayochangia kuwapo kwa migogoro ya mara kwa mara.
“Tunaamini rasilimali na mapato ya nchi yakitumika vizuri yanaweza kutekeleza mambo haya na wafanyakazi wakawa na maslahi bora,” alisema.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA