JK: Serikali italinda ardhi ya wakulima wadogo

Rais Jakaya Kikwete katika maungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa USAID Dkt.  Rajiv Shah katika hoteli ya Sheraton jijini Addis Ababa leo April 9, 2012  ambako kwa pamoja wanahudhuria Kongamano la Uchumi la Kimataifa kwa Afrika linaloshirikisha zaidi ya viongozi 700 wa nchi, biashara na uchumi kutoka sehemu mbalimbali duniani.

XXXXXXXXXXXXXXXXX
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema  kuwa miradi mikubwa ya kilimo ya kibiashara nchini itatekelezwa kwa shabaha mbili kubwa - ambazo ni kuwatoa wakulima katika umasikini na kulinda miliki ya ardhi yao.

Aidha, Rais Kikwete ameambiwa kuwa Marekani inataka kuhakikisha kuwa Mradi wa Uendelezaji Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania – Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT) unakuwa ni mfano unaong’ara wa uendelezaji kilimo katika Bara la Afrika.

Akizungumza na Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Dkt. Rajiv Shah kwenye Hoteli ya Sheraton mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Kikwete amesema kuwa shahaba kuu zaidi ya miradi kama SAGCOT ni kuwatoa wakulima wa Tanzania katika umasikini katika kipindi kifupi na kulinda miliki ya ardhi yao.

Rais Kikwete na Dkt. Shah wako mjini Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF), Kanda ya Afrika, ulioanza leo, Jumatano, Mei 9, 2012.

Rais Kikwete alikuwa anazungumzia hofu ya baadhi ya watu kuwa miradi mkubwa ya kilimo nchini itachukua ardhi ya wakulima wadogo ili iweze kufanikiwa. “Nia na madhumuni ya miradi mikubwa ya kilimo nchini siyo kuwapora wakulima wetu ardhi yao. Hasha. Nia yetu ni kuwasaidia ili wakue na watoke kwenye hali ya kilimo cha kujikimu na kuingia katika kilimo cha biashara.”

Rais amesema kuwa wakulima wakubwa watapewa ardhi tu pale ambako iko ardhi ya kutosha na hata baada ya kupewa ardhi watatakiwa kuwasaidia wakulima wadogo wanaokuwa wanaishi jirani na shamba la wakulima hao wakubwa.

“Tutawapa ardhi kubwa wakulima wakubwa pale ambako iko ardhi ya kutosha. Na hata baada ya kuwa tumepewa ardhi hiyo,  wakulima hao wakubwa watatakiwa kuwasaidia na kushirikiana na wakulima wadogo. Hii ndiyo namna pekee ya kuwasaidia wakulima wetu kuondokana na umasikini,” amesema Rais Kikwete.

Naye Dkt. Shah amemwambia Rais Kikwete kuwa Marekani imedhamiria kuhakikisha kuwa SAGCOT unakuwa mfano wa miradi ya mfano na inayong’ara katika Afrika. USAID ni moja ya mashirika ya kimataifa ambayo inashirikiana na Serikali katika kuendeleza mradi huo.

Dkt. Shah pia amemweleza Rais Kikwete kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Nchi Tajiri na Zenye Viwanda (G-8) ambao umepangwa kufanyika Marekani kuanzia wiki ijayo. Rais Kikwete ni Waziri Mkuu wa Ethiopia, Bwana Meles Zenawi ni miongoni mwa viongozi wane wa Afrika walioalikwa na Rais Barack Obama wa Marekani kuhudhuria mkutano huo.

Katika mkutano mwingine, Mtendaji Mkuu wa Benki ya HSBC, Bwana Andrew Dell amemwambia Rais Kikwete kuwa benki yake iko tayari kuiwezesha Tanzania kukopa fedha nyingi ya ujenzi wa miundombinu kwa mpango wa Sovereign Bond badala ya kutumia fedha za kodi kujenga miundombinu ambayo inaweza kujengwa kwa urahisi na kwa kutumia fedha ya benki hiyo.

Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na wakurugenzi wa Kampuni ya MSP Steel and Power Limited ya India, Mabwana Manish Agrawal na Pranay Agranal ambao wanataka kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.

Rais amewakaribisha wakurugenzi hao kuwekeza katika uchumi wa Tanzania akisisitiza kuwa Tanzania bado unahitaji wawezekezaji kwa wingi na katika sekta zote.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU