Kamati ya Lowassa yataka kutoka Nida maelezo ya vyeti feki

SIKU chache baada ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kuibua tuhuma nzito zinazoonyesha baadhi ya wanajeshi wa JWTZ na Polisi wameghushi vyeti vya elimu ili kupata ajira, Kamati ya Bunge ya  Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imetaka maelezo ya kina kutoka mamlaka hiyo kuhusiana na tuhuma hizo.

Wakati Kamati ikitaka kupata taarifa hizo, wajumbe wake wawili ambao waliwahi kuwa Mawaziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani, John Chilligati na Muhammed Seif Khatibu kwa nyakati tofauti, wametoboa siri ya jinsi walivyofanyiwa fitina na kupigwa majungu wakati wa mchakato wa mradi huo wa Vitambulisho vya Taifa, hatua iliyotokana na kuwa na fedha nono ambayo ni zaidi ya Sh200 bilioni hivyo, kukwama kuufanikisha kwa wakati.

Katikati ya mwezi huu, Nida ilitoa taarifa yake kuhusu mchakato wa uandaaji Vitambulisho vya Taifa na kusema, umekumbana na vikwazo vya awali ambavyo ni pamoja na kuwapo kwa vyeti vyenye utata katika majeshi, huku askari polisi 700 na wanajeshi wa JWTZ 248 wakiwa ni miongoni mwa askari waliobainika.
Jana, kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Edward Lowassa ilitembelea Ofisi za Nida ndipo na kutaka maelezo kuhusu tuhuma hizo ambazo zimeibua mjadala mzito nchini.

Lowassa alisema ni muhimu kamati yake ikapata taarifa kamili kuhusu vyeti hivyo kwa kuwa taarifa zilizotolewa zimegubikwa na utata.

“Tunataka tujue kuhusu hivi vyeti kwa kuwa taarifa zimetoka kwenye magazeti kuhusu majeshi ambayo ni ya ulinzi, awali zilitoka zikakanushwa, lakini tunataka tujue ukweli wake kwa undani,” alisema Lowassa.

Hata hivyo, Lowassa alimpa fursa Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dickson Maimu kuchagua ama kutoa maelezo hayo mbele ya waandishi wa habari waliokuwapo kwenye kikao hicho au baada ya waandishi hao kuondoka ukumbini.

Maimu alisema angependa kutoa maelezo ya ziada kuhusu suala hilo kwenye kikao na kamati hiyo pasipo kuwapo waandishi wa habari.

Mbali na kuhoji kuhusu suala hilo la vyeti, Lowassa na kamati yake pia walitaka vitambulisho hivyo vya taifa visimamiwe kwa umakini na visigawiwe kama njugu ili kulinda utaifa.

“Kitambulisho cha taifa ni kitu cha thamani sana hivyo ni muhimu kulinda mali zetu na muwe makini kwa watu wa mipakani mwa nchi,” alisema Lowassa na kuongeza kwamba ni muhimu Nida wakaeleza wanahitaji bajeti ya kisi gani ili kuweza kukamilisha kazi hiyo.

Khatib na Chiligati
Khatib ambaye ni Mbunge wa Uzini, alisema wakati alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, kulikuwa na fitina kubwa kwenye suala hilo na kusema hatua iliyofikiwa sasa inatia matumaini.
Pia Khatib alitaka kujua umuhimu wa vitambulisho hivyo na vile vya Zanzibar ambavyo Wazanzibari wamekuwa wakivitumia kwa muda mrefu.

Akijibu hilo, Maimu alisema vitambulisho vya Zanzibar ni vya ukaazi na hivi vya taifa ni vya utaifa hivyo, Wazanzibari wote watapaswa kuwa navyo ili kutambulika.

Kwa upande wake, Chiligati ambaye ni Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), alisema mradi huo una fedha nyingi na ndiyo maana hata yeye alipokuwa Waziri alikumbana na fitina hizo.

Alisema fitina hizo zilikuwa zinafanywa na wazabuni ambao walikuwa wakipigania kupata nafasi ya kutengeneza vitambulisho hivyo, kitu ambacho kilifanya wengine kwenda mahakamani.

Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse alitaka vitambulisho hivyo vitengenezwa kwa uimara wa hali ya juu ili vidumu kwa muda mrefu.
Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo alisema ni muhimu elimu ikatolewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa vitambulisho hivyo haraka.

Utata wa mradi
Mradi huo uliwahi kuibua utata mkubwa wakati Lawrence Masha akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, kwani ilifikia wakati kukawa na taarifa za ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 kwa ajili ya kupendelea baadhi ya kampuni.

Utata huo uliibuka mwaka 2009 baada ya kuwepo kwa shinikizo la kupendelea kampuni fulani kati ya 54 hatua ambayo Mamlaka ya Zabuni ya wizara hiyo ililazimika kuing’oa Kampuni ya Sagem Securite katika mchujo wa awali na kupitisha kampuni sita, ikiwamo Iris Corporation Berhad ya Malaysia baadaye ilishinda.

Katika mchujo huo wa awali uliofanyika mwaka 2009, kampuni zilizoingia mbali ya Iris zilikuwa ni Unisys ya Afrika Kusini, Giesecke & Devrient Fze ya India, Madras Security Printers, Marubeni Corporation ikishirikiana na Zetes pamoja na Nec za Japan na Tata Consultancy Services ambayo ilishirikiana na Ontrack Innovations Ltd ya India.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*