MAWAZIRI WA KIKWETE WATISHANA

HALI ya utendaji kazi ndani ya Baraza la mawaziri imeendelea kuwa tete baada ya mmoja wa mawaziri waandamizi kumpa mwenzake muda wa siku saba kutekeleza matakwa yake, vinginevyo watafikishana mbali.
Akiwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa barabara kwa ajili ya mabasi yaendayo kasi, na daraja lililopo eneo la Tangibovu jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, alimshambulia hadharani Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo na kutishia kumshitaki kwa Rais Kikwete ikiwa hataruhusu kutolewa kwa vifaa vya ujenzi, mali ya Kampuni ya Strabag ya Ujerumani vilivyozuiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Lakini Waziri Mkulo aliiponda kauli ya Waziri Magufuli, akidai kuwa amekwenda kinyume cha utaratibu wa kazi kwa kutishana kupitia magazetini, na kwamba namna pekee ilikuwa kufuata taratibu.

Akizidi kuishutumu Wizara ya Fedha, Magufuli alidai kuwa hawezi kubebeshwa lawama za kuchelewa kwa ujenzi wa barabara hiyo, na hatakubali kuadhibiwa kwa uzembe na makosa ya watendaji wengine wa serikali.
Kauli ya Magufuli ilikuja baada ya kukuta kazi za ujenzi zimesimama, na ndipo Meneja wa kampuni hiyo ya ujenzi, Frank Rohde, akamweleza kuwa kuna vifaa yakiwamo makatapila vimezuiliwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo fedha.
“Hili ni agizo la rais mwenyewe kuhusu upanuzi wa barabara hizi ili foleni ziishe na waziri analifahamu, nitaongea naye kama akishindwa basi nitamchongea kwa rais, Mamlaka ya Mapato (TRA) nayo nitaongea nayo,” alisema.
Imebainika kuwa kampuni hiyo inaidai serikali fedha nyingi kama gharama za ujenzi, lakini katika namna ya kushangaza wamezuiliwa kuchukua vifaa vyao bandarini kwa madai ya kutolipa ushuru.
“Kilichobaki sasa ni kuchongeana kwa Rais Kkwete ili mambo yaende vizuri, na ili kufanikisha ujenzi huo ni lazima kila mmoja atimize wajibu wake,” alisema.
Alisema kampuni hiyo ya Ujerumani inakwenda na muda ili kumaliza mradi kwa wakati, hivyo hawataki kupewa vikwazo vyovyote.
Kwa mujibu wa waziri, mradi huo unajengwa kwa manufaa ya wakazi wa Dar es Salaam, kwa kuwa utapunguza foleni kwenye jiji, lakini pia utakuwa ni mkombozi kwa taifa, hivyo ni mradi wa wote, hivyo hautakiwi kupewa vikwazo vyovyote vikiwamo vya wizara, Tanesco au TRA.
Alifafanua kwamba kampuni hiyo inatakiwa kukaa kwenye eneo la ujenzi kwa muda wa miezi 36 na Wajerumani wanajua jinsi ya kujali muda, kwani hatua ya kupewa vikwazo kwa kampuni hiyo, inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi wenyewe.
Magufuli alilipa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) siku saba kun’goa nguzo za umeme kando kando ya barabara hiyo, na endapo watashindwa atazing’oa kwa nguvu.
Waziri huyo pia aliwataka wananchi waliojenga eneo la barabara kubomoa makazi yao haraka iwezekanavyo, na wasidanganywe na mtu ikiwa ni pamoja na kwenda mahakamani, kwani hata wakichukua hatua hiyo hawana uhakika wa kushinda.
Alielezea kuwa mradi wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi eneo la Kimara hadi Kivukoni utagharimu sh bilioni 288, ambapo ujenzi wa barabara pekee utagharimu sh bilioni 240 na vituo vyake kugharimu sh bilioni 44.
Alisema hata kama mabasi hayo yatashindwa kuletwa nchini, barabara hizo zitatumika kwa magari ya wananchi, ambapo mradi huo ukikamilika Barabara ya Morogoro itakuwa na njia nane.
Mkulo: Sijui kitu
Akihojiwa na Tanzania Daima kwa njia ya simu, Waziri Mkulo, alishangazwa na mashambulizi dhidi yake akidai kuwa hajui lolote na kwamba kitendo hicho cha Magufuli ni kinyume cha taratibu za kazi.
“Si utaratibu kwa waziri kuzungumza kwenye magazeti eti kusema atanishitaki kwa rais, kuna utaratibu wake… huo si utaratibu,” alisema Mkulo.
Kadhalika alidai kuwa haelewi jambo lolote kuhusiana na kampuni hiyo, na hivyo hawezi kuzuia malipo wala kutolewa kwa mizigo yake bandarini na kwamba anayewajibika kuelewa masuala hayo ni katibu mkuu wa wizara.
Jitihada za kumpata katibu mkuu wa wizara hiyo zilishindikana, na hata alipotafutwa Msemaji wa Wizara ya Fedha, Namsembaeli Mduma, simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI