MNYIKA AMBWAGA NG'UMBI-MAHAKAMA KUU

Baadhi ya wafuasi wa Chadema wakiwa nje ya jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania leo asubuhi katika kesi ya kupinga matokeo ya Ubunge iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Hawa Ng'umbi.
Mbunge wa Ubungo John Mnyika akishuka katika gari yake Mahakamani.
Mbunge wa ubungo John Mnyika katikati akiingia Mahakamani
Baadhi ya Waandishi wa Habari
Baadhi ya wafuasi wa CCM wakiwa Mahakamani.Kwa hisani ya Habari Mseto Blog
Ng'umbi kama anasema, "Sina ugomvi na wewe ni Siasa tu"

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akipeana mkono na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Baada ya kutolewa kwa hukumu na Jaji Upendo Msuya wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wapenzi na mashabiki wa Chadema walilipuka kwa furaha.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akiwa amebebwa juu juu na wafuasi wa chama chake.

HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemtangaza Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), kuwa ndiye mbunge halali wa jimbo hilo na matokeo ya uchaguzi ya jimbo hilo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Novemba mwaka 2010, yalikidhi matakwa ya kisheria.
Uamuzi huo ulisababisha jiji la Dar es salaam kuzizima kwa shangwe na nderemo na baadhi ya barabara kufungwa kwa muda kutokana na umati mkubwa wa wafuasi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wakishangilia ushindi wa mbunge huyo.
Akisoma hukumu hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa shauku kubwa ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na maelfu ya wafuasi wa vyama hivyo, Jaji Upendo Msuya alitupilia mbali hoja moja baada ya nyingine, kabla ya kuhitimisha na kufutilia mbali pingamizi lililowekwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Hawa Ng’umbi.
Akichambua dai la kwanza, la kwamba mdaiwa wa pili (Mnyika) aliingiza laptop binafsi katika chumba cha kujumlishia kura ambazo zilimuongezea kura hewa14,857 ambazo hazikuhesabiwa, jaji huyo alisema mashahidi watatu wa mlalamikaji walishindwa kuthibitisha dai hilo katika ushahidi wao.
“Hoja katika dai hili ni je laptop hizo zilitumika kuongezea kura au la..lakini mahakama baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili umeona Ng’umbi ameshindwa kutoa vielelezo au kuleta ushahidi wa kuunga mkono dai lake kwamba kompyuta hizo mali ya Mnyika ambazo kisheria hazikupaswa kutumika kujumlishia kura, zilitumika na kwa sababu hiyo mahakama hii inatupilia mbali dai hilo,” alisema Jaji Msuya.
Kuhusu hoja ya kura 14,857 zinazodaiwa kuwa hewa, jaji huyo alisema amelazimika kuzifanyia mahesabu idadi ya kura walizopata ambapo alisema Mnyika alipata kura 66,742, Ng’umbi 50,554 jumla ya kura hizo ni 117,286 na wagombea wengine 14 toka vyama vingine walipata kura 15,210 kwa hiyo jumla ya kura zote walizopigiwa wagombea wote 16 ilikuwa ni 132,496.
“Kura 14,857 zinazobishaniwa na mdaiwa zinaweza kuhesabiwa kwa jumla ya wagombea 16 ambao walipata 132,496 ambapo kura halali zilizopigwa ni 117,639, kura zilizoharibika ni 2,184 na unapata jumla kura 14,857.
Alisema baada ya kufanya hesabu ya kura hizo alibaini kuwepo kwa tofauti ya kura 353 sawa na asilimi 0.3 ya jumla ya kura halali zilizopigwa.
“Katika akili yangu nimetafakari dai hili, pia nimezingatia mazingira ya kujumlishia kura yaliyoelezwa na pande zote katika kesi hii, nimezingatia muda wa kazi na kielelezo kilicholetwa na upande wa utetezi ni sahihi na dosari ya kura 14,857 haikuweza kufanywa na laptop hizo na Mnyika hakupinga kuingia nazo kwa ajili ya kuhakiki kura ambazo zilishahesabiwa na maofisa wa NEC .
“Kwa maelezo hayo hapo juu mahakama hii inasema hata sheria haikatazi wakala wa mgombea kuingia na laptop kwenye chumba cha kujumlishia kura na pia Ng’umbi ameshindwa kuleta wataalamu wa kompyuta waje kutoa ushahidi ambao ungeonyesha laptop hizo zilitumika kujumlishia kura na kwa maana hiyo ombi hilo nimelikataa,” alisema Jaji Msuya.
Kuhusu dai kuwa Mnyika aliingiza watu zaidi ya nane ambao hawakustahili katika chumba cha kujumlishia kura, jaji huyo alisema Ng’umbi ameshindwa kutoa ushahidi na hata kama waliingia waliathiri vipi taratibu na kanuni za uchaguzi wa jimbo hilo.
Kuhusu dai la Mnyika kwamba alimkashifu Ng’umbi katika mkutano wake wa hadhara alioufanya Septemba mwaka 2010 na kudaiwa alimuita ni fisadi kwa sababu aliuza nyumba za UWT, alisema pia mlalamikaji huyo ameshindwa kuthibitisha dai hilo kwani lilijikita katika misingi ya ushahidi wa kusikia ambao hautakiwi mahakamani.
“Kwa kuhitimisha mahakama hii imetupilia mbali madai yote ya mlalamikaji na kwa kauli moja inamtangaza Mnyika kuwa ndiye mbunge halali wa jimbo la Ubungo na kwamba taratibu zote za uchaguzi zilifuatwa,” alimaliza Jaji Msuya na kusababisha kulipuka kwa nderemo na vifijo toka kwa wafuasi wa CHADEMA.
Ng’umbi aondoka kwa huzuni
Muda mfupi baada ya kutolewa kwa hukumu, mlalamikaji katika kesi hiyo, Hawa Ng’umbi, aliondoka mahakamani hapo kwa huzuni huku akisindikizwa na baadhi ya wanachama wa CCM waliofika hapo kusikiliza kesi hiyo.
Akizungumzia kama ana nia ya kukata rufaa, Ng’umbi alisema bado anatafakari ili aweze kupata majibu kama atakata rufaa ya kupinga hukumu hiyo.
Alisema atakaa na uongozi wa juu wa chama chake kwa ajili ya kuangalia kama kutakuwa na uwezekano wa kufanya hivyo, haraka iwezekanavyo.
‘Hadi sasa siwezi nikasema lolote juu ya kukata rufaa, lakini nitatolea ufafanuzi juu ya hilo pindi nitakapokaa na uongozi wa juu na kulijadili suala hilo,’ alisema Ng’umbi.
Katika kesi hiyo Ng’umbi alitetewa na wakili wa kujitegemea Issa Maige, wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitetewa na wakili Kiongozi wa Serikali Justus Mulokozi. Mnyika alitetewa na Edson Mbogoro.
CHADEMA yafanya kufuru
Baada ya kumalizika kusomwa kwa hukumu hiyo, maelfu ya wanachama wa CHADEMA walimbeba juujuu Mnyika na kumtoa nje ya viwanja vya mahakama kwa shangwe.
Wabunge wawili wa chama hicho, Ezekiel Wenje wa jimbo la Ilemela na Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa mjini waliungana na umati huo na ndipo ukaanza msafara wa kuelekea katika ofisi za jimbo la Ubungo huku wakiimba nyimbo mbalimbali za kusifu hukumu hiyo.
Msafara ulipitia barabara ya Maktaba, Bibi Titi, Morogoro ambapo polisi waliokuwa wametanda kila eneo la mji, walijaribu kumzuia Mnyika wakitaka apande gari kuepusha msongamano, lakini wananchi waligoma na kutishia kufanya fujo hali iliyowalazimu askari kuusindikiza kwa amani.
Idadi ya watu ilikuwa ikiongezeka kila baada ya muda, na baadhi ya wafanyakazi na wenye biashara zao waliacha kwa kwa muda na kuungana na wafuasi hao kushangilia.
Katika eneo la Magomeni Mwembechai wanafunzi wa Shule ya Msingi Dk. Omar waliungana na msafara huo sambamba na wanafunzi wengine wa shule mbalimbali za sekondari na katika eneo la soko la Big.
Brother wafanyabiashara walionekana wakiwa wamejipanga barabarani na kupunga mikono juu huku wakiwa wameshika bendera za CHADEMA.
Hata hivyo, mamia ya watu katika eneo la Kituo Kikuu cha Mabasi walimzuia Mnyika wakitaka aingie ndani ya stendi hiyo kuhutubia jambo ambalo lilipingwa na viongozi wa chama hicho kwa kuhofia uvunjifu wa amni.
Mnyika auhutubia
Akiwa katika eneo la ofisi za CHADEMA, Ubungo, Mbunge huyo alilazimika kuhutubia umati wa watu, ambapo alisema hukumu hiyo ni ushindi wa wananchi wote dhidi ya ufisadi unaofanywa na serikali ya CCM.
“Kwa sababu ya mfumo wa serikali yetu nilijua leo (jana) ingekuwa ni mwisho wa ndoto yangu ya kuwatumikia wananchi, lakini kwa sala zenu tumeshinda na sasa ni fursa nyingine ya kuwatumikia ninyi mlionituma pasipo kuwa na kizuizi chochote,” alisema Mnyika na kushangiliwa.
Alisema mazingira ya kazi awali yalikuwa magumu kutokana na muda mwingi kufuatilia kesi mahakamani na kwamba sasa ana uhakika wa kuongeza nguvu juu ya kuzisemea shida za wananchi bungeni na hata kuzitatua.
Aliitaka Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iwaeleze wananchi hatua waliyofikia baada ya aliyekuwa mshindani wake Hawa Ng’umbi kuwahi kukamatwa na taasisi hiyo kwa makosa ya rushwa.
Alisisitiza kuwa ni wakati wa wananchi kujua nini kinaendelea dhidi ya kesi hiyo na kwamba wasimuonee aibu kwa kuwa anatoka chama kinachotawala.
Akizungumzia masuala ya kitaifa Mnyika alisema anazo nyaraka zinazoonyesha matumizi mabaya ya fedha katika Benki Kuu huku akisema hali hiyo inaiweka nchi katika hatari ya kukwama kiuchumi kutokana na ufisadi unaofanyika.
“Ninazo nyaraka za siri za Benki Kuu na ninatarajia kuziweka hewani muda wowote kuanzia sasa pale panafanyika ufisadi wa kutisha hali inayofanya mfumko wa bei kuongezeka kila siku,” alisema Mnyika.
Kuhusu tatizo la maji katika jimbo la Ubungo na madudu ya wizara hiyo, alisema ataenda kupambana naye bungeni baada ya kuonyesha kiburi cha kutosikia kilio cha wananchi huku akisisitiza suala la Machinga kulifikisha bungeni
Mbowe: Ni ushindi wa Watanzania
Naye Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amesema ushindi wa Mnyika ni wa wananchi wa jimbo la Ubungo, wanachama na Watanzania kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mbowe alisema kesi za uchaguzi zinagharimu kiasi kikubwa cha fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya shughuli zingine za maendeleo, hivyo suala hilo litawasilishwa bungeni kujadiliwa.
Mbowe alisema pesa za uchaguzi zinazopotea zingeweza kutumika kwa ajili ya kununua dawa hospitali, vitanda na madawati kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
“Wananchi kama mlivyoona wenzetu walikuwa na mashtaka matano, ambayo yametupiliwa mbali na jaji kutokana na kukosa uthibitisho, kukimbilia mahakamani kunakofanywa na baadhi ya wabunge huku wakikosa vielelezo, sio kuzuri,” alifafanua.
Alisema kama Mnyika angepoteza ubunge huo, ni wazi kwamba wananchi wasingepata mwakilishi mwenye uwezo kama wake.


juu

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU