MTEULE WA RAIS AUOTA URAIS

WIKI mbili baada ya Stephen Maselle (pichani) kuapishwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, mteule huyo wa Rais Jakaya Kikwete amerejea jimboni kwake kuzungumza na wapiga kura na kuwaambia kuwa ipo siku atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.Wakati Masele akitoa kauli hiyo, naibu mwenzake katika wizara hiyo ya Nishati na Madini, George Simbachawene amesema atafanya kazi usiku na mchana ili asimwangushe Rais Kikwete aliyemteua na Watanzania kwa ujumla.

Juzi, Maselle akiwa katika mkutano wa hadhara Mjini Shinyanga uliohudhuriwa na makada mbalimbali wa CCM akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho wa Mkoa, Khamis Mgeja, alitangaza ndoto hiyo akisema ipo siku atachaguliwa kuwa mkuu wa nchi akirejea historia ya Rais Kikwete.

Alifafanua kwamba Kikwete aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, akapanda hadi kuwa Rais wa nchi jambo ambalo hata yeye linampa matumaini ya kufikia nafasi hiyo.

“Unajua Mheshimiwa Rais (Kikwete) alianzia kukaa kwenye wadhifa na kiti ambacho leo mimi ndiyo nakikalia, hivyo baadaye nitakuwa kama yeye, nitunzeni nidumu ili baadaye nami nije kuwa kiongozi mkubwa wa nchi hii (Rais),” alisema huku akishangiliwa na wanachama hao wa CCM.Maselle alisema Rais Kikwete alianza kwa wadhifa wa unaibu waziri na baadaye akawa waziri kamili na leo ni kiongozi wa nchi, hivyo naye anafuata nyayo zake.

Katika hotuba yake, alitumia aya za kwenye Biblia kujinasibu na kujifananisha na manabii waliokuwa wakisubiriwa kuwakomboa wanadamu katika zama mbalimbali, ikiwamo zama za Nabii Musa.Alisema kama ilivyokuwa Musa ambaye Mungu alimchagua kuwakomboa wana wa Israel, yeye ni nabii aliyetumwa kuwakomboa wana Shinyanga na Watanzania kwa ujumla.

Maselle ambaye ni Mbunge wa Shinyanga Mjini, alisema alikuwa na subira kama Nabii Ayub, wakati Rais Kikwete anapanga Baraza lake la Mawaziri la kwanza ambalo yeye hakuwapo na kuongeza: “Sikuwa na wasiwasi, nilijua ipo siku nitateuliwa, hivyo nilichofanya ni kuwa na subira kama Nabii Ayubu.”
Aliwataka wakazi wa Mkoa wa Shinyanga kumuunga mkono katika utekelezaji wa majukumu yake ya sasa katika wadhifa alionao ili shughuli zake ziwe za mafanikio.

Akizungumza katika mkutano huo, Mgeja alimtaka Maselle ambaye anashughulikia masuala ya madini, kuhakikisha anamaliza kero za wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya migodi, zinazofanywa na wawekezaji katika sekta hiyo hasa katika Wilaya za Kahama na Kishapu.

Alisema katika sekta hiyo kuna migogoro mingi ambayo imekuwa kero kubwa kwa wananchi hivyo kumtaka awe na uchungu wa kuwasaidia kwa dhati wananchi hasa wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakifukuzwa mara kwa mara machimboni kupisha wawekezaji.

Simbachawane
Kwa upande wake, Simbachawene juzi aliwaambia Watanzania kuwa atafanya kazi usiku na mchana ili kutimiza matarajio yao kutokana na kuwa wengi wamepoteza imani na wizara hiyo.Alikiri kuwa wizara aliyopewa ni ngumu na ina changamoto nyingi zaidi kuliko maeneo mengine kutokana na dunia kuwa ya utandawazi.

Akizungumza na umati wa wananchi waliofurika katika Viwanja vya Kibakwe waliojitokeza kumpongeza Mbunge wao wa Kibakwe kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo, Simbachawene alisema katika siku tatu alizokaa ofisini kwake alibaini kuwa wizara hiyo ina changamoto kubwa zinazohitaji mtu mwenye wito katika kukabiliana nazo.

“Ndugu zangu, hata Yesu hakuwaridhisha watu wote na mimi nasema siwezi kuwaridhisha kwa asilimia 100 lakini sitakubali kushika mashavu kwa huzuni lazima nitalinda heshima kubwa niliyopewa na Rais na Watanzania wenzangu, nasema nitapambana kufa na kupona hadi kieleweke, muhimu nawaomba mniombee kwa Mungu,” alisema Simbachawene.

Naibu Waziri huyo anayeshughulikia nishati, alisema hatakubaliana na uovu wa aina yoyote katika ofisi yake ambao mwisho wa siku utamfanya apate huzuni kwani mpango wa sasa serikalini ni kuwa kila anayekosea dawa yake ni kutimuliwa.

Simbachawene alisema siku tatu alizokaa katika ofisi yake amebaini kuwa kazi iliyoko mbele yake ni kubwa kuliko alivyotarajia.

Akizungumzia namna atakavyoitumikia nafasi hiyo mpya pamoja na majukumu ya jimbo, Simbachawene aliwataka wapiga kura wake kukubaliana na wazo la Rais ili aitumikie nafasi hiyo kwa Watanzania na akaomba wakubali kuwa sasa hataonekana mara nyingi jimboni kama walivyokuwa wamezoea kumuona.

“Kwa sasa siwezi kuonekana mara nyingi kama ilivyokuwa hapo awali, lakini nawaahidi kuwa nitakuja msihofu sana. Pengine niwakumbushe kuwa sasa mimi nimekuwa ni sehemu ya dola hivyo zile simu za utani kutoka jimboni naomba zipungue na tena simu nipigiwe majira ya jioni.’

Kwa upande wake, Mbunge wa Mpwapwa (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory Teu alisema watafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa kuiletea Wilaya ya Mpwapwa maendeleo ya kweli.
Teu ambaye kabla ya uteuzi wa hivi karibuni alikuwa Naibu Waziri wa Fedha, aliwaambia wananchi kuwa amefurahishwa kuteuliwa kwa Simbachawene.


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU