MWANASHERIA MKUU AFAFANUA UTEUZI WA WABUNGE NA MAWAZIRI WAPYA

Dar es Salaam, Tanzania
Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 4 Mei, 2012 alitangaza
mabadiliko katika safu ya Baraza la Mawaziri. Katika uteuzi wa Mawaziri na
Manaibu Waziri, Mheshimiwa Rais aliwateua Mawaziri wapya kutoka miongoni mwa
Wabunge aliokuwa amewateua na kuwatangaza. Baada ya uteuzi huo, kumetolewa
maoni kwamba hatua ya Mheshimiwa Rais kuwateua Wabunge Wapya ambao hawajaapishwa
Bungeni kuwa Mawaziri ni kitendo cha uvunjaji wa Katiba.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayachukulia maoni haya kama
ni jambo lenye maslahi ya jamii na linalohitaji kufafanuliwa; kwa upande mmoja
lakini pia, kutolewa kwa elimu ya Umma; kuhusu Mamlaka ya Rais ya uteuzi wa
Wabunge.

Msingi wa Katiba tunaoanza nao ni maelekezo ya masharti yaliyomo
kwenye Ibara ya 55(4) kwamba:
“Mawaziri na Naibu Mawaziri wote watateuliwa kutoka miongoni mwa
Wabunge”
Pili, ni mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wabunge aliyopewa na masharti
ya Ibara ya 66(1)(e) yenye aina ya Wabunge wasiozidi kumi watakaoteuliwa na Rais
kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizotajwa katika aya za (a) na (c) za
ibara ya 67 na angalau Wabunge watano kati yao wakiwa Wanawake. Wabunge
aliowateuwa Mheshimiwa Rais wanatokana na Ibara hii.

Tatu, baada ya hatua zote hizi ikumbukwe kwamba aliyeteuliwa au
kuchaguliwa kuwa Mbunge anakuwa Mbunge ama baada ya kutangazwa na Msimamizi wa
Uchaguzi; au baada ya kuteuliwa na Tume ya Uchaguzi kwa wale Wabunge wa viti
maalum au anapochaguliwa na Baraza la Wawakilishi au anapoteuliwa na Rais
akitumia Mamlaka yake ya uteuzi yanayotokana na Ibara ya 66(1)(e). Hivyo Wabunge
wanaohusika hawahitaji kuapishwa kwanza Bungeni ili wawe Wabunge. Kiapo cha
Mbunge Bungeni kinamwezesha tu kushiriki katika shughuli za Bunge.

Katiba ya nchi haiweki kwa Rais masharti kwamba kabla ya kumteua
Mbunge wa aina hiyo kuwa Waziri au Naibu Waziri Mbunge huyo awe ameapishwa
Bungeni kwanza. Masharti mawili muhimu na ya kuzingatia ni kwamba mteule wa
nafasi ya uwaziri au Naibu Waziri hatashika madaraka yake ila mpaka kwa mujibu
wa Ibara ya 56 ya Katiba, awe ameapa kwanza mbele ya Rais kiapo cha uaminifu na
pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa
kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge. Sharti la pili, litahusu kiapo cha
Uaminifu katika Bunge kabla Mbunge hajaanza kushiriki katika shughuli za Bunge
kwa masharti ya Ibara ya 68 ya Katiba. Viapo hivyo havitegemeani na vinaweza
kufanyika kwa nyakati tofauti.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inasisitiza kwamba Wabunge
ambao hawajaapishwa ndani ya Bunge ni Wabunge na wanapoteuliwa kushika nafasi ya
Uwaziri au Naibu Waziri ni halali kwa kuwa uteuzi huo haukiuki masharti yoyote
ya Kikatiba au Sheria. Aidha, katika kutekeleza madaraka ya kazi ya Uwaziri au
Naibu Waziri Mbunge atahitaji kiapo mbele ya Rais hata kama hajaapishwa
Bungeni. Busara ya uandishi wa Katiba na Sheria imetambua kwamba kunaweza
kukatokea uteuzi wa aina hiyo wakati Bunge limeahirishwa kama ilivyo sasa.
Masharti ya Ibara ya 68 ya Katiba yatazingatiwa katika kikao cha Bunge
kijacho.

Bila shaka ufafanuzi huu utaleta uelewa katika jambo hili na kuepusha
mikangayiko isiyokuwa ya lazima.



Imetolewa na Jaji
Frederick M. Werema (Mb)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
06 Mei, 2012

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI