NCHUNGA: TUTAFUKUZA WACHEZAJI WENGI, TUMEGUNDUA HUJUMA
Nahodha wa Yanga, Nsajigwa Shadrack akijaribu kumdhibiti Emmanuel Okwi wa Simba katika mechi ya jana. |
UONGOZI wa Yanga umesema kwamba umepata
taarifa za awali, ya kuwa, mechi yao ya jana dhidi ya mahasimu wao wa jadi,
Simba waliyofungwa mabao 5-0, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuna baadhi ya
wachezaji walihujumu timu.
Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharragu
Nchunga ameiambia mchana huu kwamba, kufuatia taarifa hizo, Kamati
ya Ufundi inakutana leo jioni na benchi la Ufundi kujadili zaidi na pia
kuandaa taarifa nzima ya msimu.
Nchunga alisema baada ya Kama ya Ufundi kwa
pamoja na benchi la Ufundi kukamilisha taarifa hiyo, wataiwasilisha kwa Kamati
ya Utendaji, ambayo nayo itakutana kesho kujadili kwa kina ili kuchukua hatua.
“Kuna uwezekano tukawafukuza wachezaji
wengi sana, yaani sisi watu wa Yanga ni wa ajabu sana, sijui Uyanga wetu ukoje,
nashindwa hata kuelewa,”alisema Nchunga.
Nchunga alisema Waandishi wa Habari wenye
kutaka ukweli zaidi juu ya hujuma hizo wanaweza kumfuata kipa, Yaw Berko na
kumdadisi kwa nini aligoma kuendelea na mechi.
Berko hakurejea uwanjani baada ya dakika 45
za kipindi cha kwanza, Yanga ikiwa nyuma kwa bao 1-0 na nafasi yake ikachukuliwa
na kipa wa tatu, Said Mohamed aliyetunguliwa mabao manne.
“Berko aligoma kuendelea, alisema anaomba
atoke na hakuwa ameumia wala nini, alisusua tu, unajua yule ni mlokole safi,
ila baada ya kesho kila kitu kitajulikana,”alisema Nchunga.
Alipotakiwa kuwataja baadhi ya wachezaji
wanaohusishwa na tuhuma hizo, Nchunga alisema; “Siwezi kusema chochote, ila kwa
sasa unaweza kuangalia tu uchezaji wa mtu kwenye mechi ya jana na ukapata jibu.
Yanga kama Yanga itatoa taarifa rasmi baada ya taratibu zote kukamilika na
wachezaji wahusika kuitwa kuhojiwa sambamba na kuonyeshwa ushahidi ambao hadi
sasa tumekwishaukusanya,”alisema.
Yanga jana ilifungwa 5-0 na wapinzani wao
wa jadi, Simba waliotawazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu kwa kumaliza ligi
wakiwa na pointi 62.
Simba ilipata mabao yake kupitia kwa,
Emmanuel Okwi dakika ya kwanza na Patrick na 65, Mafisango dakika ya 58 kwa penalti,
Juma Kaseja kwa penalti pia dakika ya 69 na
Felix Sunzu kwa penalti dakika ya 74.
Wakati Simba ikimaliza na pointi zake 62, Azam
imekuwa ya pili kwa pointi zake 56 baada ya jana kuifunga Kagera Sugar mabao
2-1 Uwanja wa Chamazi na Yanga imeshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 49.
Mwaka 1977, baada ya Yanga kufungwa 6-0 na
Simba ilivunja timu na kuunda kikosi kipya, ambacho kilirejesha heshima ya
klabu.
Mwaka 1994, Yanga ilifungwa 4-1 na Simba na
baada ya mchezo huo, ilivunja tena kikosi kutokana na tuhuma za kuhujumiwa na
wachezaji wake, safari hiyo ikidaiwa aliyekuwa mfadhili mmoja wa klabu hiyo
mwenye asili ya Kiasia, aliwapa fedha wachezaji wafungwe ili kuwakomoa viongozi
katika vita iliyokuwa inaendelea baina yao.
Baadhi ya wachezaji waliobakishwa kikosini
walikuwa ni Kenneth Mkapa, Constantine Kimanda, Sekilojo Chambua, Sanifu Lazaro
‘Tingisha’ na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, wengine wote akiwemo kipa Steven
Nemes, Said Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) walitimuliwa kwa tuhuma hizo.
Baada ya hapo, Yanga iliundwa na wachezaji
waliokuwa wakiandaliwa na Tambwe Leya (sasa marehemu) katika kikosi cha pili,
ambao ni pamoja na Godwin Mashoto (sasa marehemu), Mzee Abdallah, Anwar Awadh,
Maalim Saleh ‘Romario’, Nonda Shaaban na wengineo, waliosajiliwa kutoka timu
mbalimbali kuimarisha kikosi kama Bakari Malima, Reuben Mgaza waliotoka Pan
African.
Kipigo cha sasa cha Yanga kinakuja katika
mazingira sawa na kipigo cha 1994, kwani klabu inakabiliwa na mgogoro na baadhi
ya viongozi wa zamani wa klabu hiyo na kundi la Wazee la klabu hiyo kuwa kwenye
vita ya kumng’oa Nchunga madarakani.
Comments