TANESCO KUKOPESHWA SH. BILIONI 408

SERIKALI imekubali kulidhamini Shirika la Umeme nchini(Tanesco) ili liweze kupata mkopo wa Sh408 bilioni utakaosaidia shirika hilo kujiendesha.

Kufikiwa kwa uamuzi huo wa serikali kutamaliza mvutano uliokuwapo kati ya Bodi ya Tanesco na Wizara ya Nishati na Madini ambao ulisababisha Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Jenerali Mstaafu Robert Mboma kumwandikia aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja akihoji sababu za kutokutekelezwa kwa agizo la Rais Jakaya Kikwete la kulipatia shirika hilo Sh408 bilioni kwa ajili ya kujiendesha.

Barua ya Mboma ya Machi 20, mwaka huu kwenda kwa Ngeleja, ambayo gazeti hili ilifanikiwa kuiona, ilisema mnamo Machi 8, mwaka huu, Rais Kikwete aliagiza Tanesco ipewe haraka mkopo wa Sh408 bilioni lakini akasema hadi sasa amri hiyo ya Amiri Jeshi Mkuu haijatimizwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkurugenzi mtendaji wa Tanesco, William Mhando alisema , sasa mkopo huo uko mbioni kupatikana.

Mhando alisema mpaka sasa bado hawajapata mkopo huo lakini wako kwenye mazungumzo ya mwisho ya kuupata baada ya serikali kukubali kutoa dhamana yake.

"Ndiyo tunamalizia mazungumzo ili tuweze kupata mkopo na serikali imeshakubali kutudhamini kilichopo sasa ni kubadilishana nyaraka na Citi bank," alisema Mhando.

Kuhusu hali ya umeme nchini Mhando alisema, maji yaliyopo hivi sasa yanaweza kusaidia umeme upatikane hadi Agosti mwaka huu.

Alisema kutokana na mvua kutonyesha kwa wingi katika bwawa kama la Mtera lina maji kidogo na limebakia mita 1.36 kufikia mwisho.

"Bwawa la Mtera linatakiwa liwe na mita za ujazo 698.5 na sisi tunaruhusiwa kutumia hadi kufikia mita 690.0 hivi sasa liko na mita za ujazo 691.36 hivyo tumebakiwa na mita 1.36 ambazo ni kidogo," alisema Mhando.

Mhando alisema shirika hivi limeweza kukusanya kiasi cha Sh60 bilioni kutoka serikalini kati ya Sh86 bilioni walizokuwa wakizidai.

Wakati huohuo mtambo wenye uwezo wa kufua umeme wa megawati 50 wa kampuni ya Symbion Power uliofungwa mkoani Arusha unatarajiwa kuanza kazi katika wiki mbili zijazo katika mpango wa ubia katika ya sekta za umma na binafsi wenye lengo la kulinasua taifa kutokana na upungufu wa nishati ya umeme.

Akithibitisha taarifa hizi jana, Ofisa mtendaji mkuu wa Symbion Power, Paul Hinks alisema kwamba, ujenzi wa mtambo huo wa kuzalisha megawati 50 mjini Arusha umeshakamilika na kwamba kampuni yake ilikuwa inamalizia tu maunganisho katika gridi ya taifa kabla mtambo haujaanza kazi.

“Mtambo utaanza kufanya kazi katika wiki mbili zijazo au mapema zaidi …….hivyo ndivyo nionavyo kwa sasa,” mkuu huyo wa Symbion alisema.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU