TASWA YAMLILIA MWANAHABARI RACHEL MWILIGWA ALIYEFARIKI USIKU WA KUAMKIA JANA


CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinaungana na familia na wanahabari wote nchini kuomboleza kifo cha Mhariri wa Habari za Michezo wa gazeti la Mtanzania Rachel Mwiligwa.
TASWA imeshtushwa taarifa za kifo cha Rachel kilichotokea usiku wa kuamkia leo, hivyo tunatoa pole kwa familia yake, waandishi wa habari za michezo na wafanyakazi wenzake wote, wasanii na wanamichezo wengine katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mdau mkubwa wa michezo na burudani.
Kutokana na msiba huo, chama kinaandaa taratibu zake za kuwasilisha rambirambi kwa namna tulivyojiwekea, kwani marehemu hadi mauti yanamkuta alikuwa mwanachama mtiifu wa TASWA. Hivyo upo utaratibu kama mwenzetu akitangulia mbele ya haki namna gani tunatakiwa tufanye.
Lakini pia upo utaratibu mwingine nje ya chama ambao utahusu mtu binafsi kuwasilisha michango ya rambirambi, ambapo TASWA inawasiliana na wahariri wote wa habari za michezo wasaidie kukusanya michango ya rambirambi kwenye vyombo vyao, ambayo wataiwasilisha kwa wajumbe wa Kamati Maalum ya kusimamia jambo hili.
Wajumbe hao ni Angela Msangi  ambaye atakuwa Mratibu akisaidiwa na Mwani Nyangasa, ambao watashirikiana na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TASWA, George John ambaye ni Katibu Msaidizi wa TASWA, Grace Hoka na Alfred Lucas ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Tunaomba ushirikiano wa wadau katika kufanikisha jambo hili.

Msiba kwa sasa kwa mujibu wa taarifa za awali upo Manzese Tiptop,tutaendelea kujulishana kadri zitakavyopatikana taarifa mpya.
Tunaomba waandishi wa habari za michezo, wasanii na wanamichezo kwa ujumla tumuenzi Rachel kwa masuala mbalimbali aliyokuwa akiyatilia mkazo ikiwemo kusimamia ukweli kwa kile alichokiamini na ndio maana tunasema tutaendelea kumkumbuka daima. Mungu amuweke mahali pema peponi. Amin
 Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*