WACHEZAJI TAIFA QUEENS WAPEWA KITITA CHA SH. MILIONI MOJA


 
*Yailaza Botswana 32-23, yatwaa ubingwa wa pili
 
MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda ametimiza ahadi aliyoitoa kwa timu ya Taifa ya Netiboli (Taifa Queens) ya kuwapa sh. milioni moja kila mchezaji endapo wangetwaa ubingwa wa Kombe la Mashindano ya Afrika ambayo yamemalizika jana jijini Dar es Salaam.
 
Mama Pinda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kuisaidia Taifa Queens Ishinde, alitimiza ahadi hiyo jana usiku (Jumamosi, Mei 12, 2012) katika hafla fupi ya kuwakabidhi wachezaji hao bankers’ cheques zao. Wachezaji 16 walipatiwa sh. milioni moja kila mmoja, na maafisa sita wa timu walipewa sh. 800,000 kila mmoja. Jumla ni sh. milioni 20.8/-
 
Akizungumza na wachezaji hao, viongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), na baadhi ya Wake wa Viongozi ambao ni wanachama wa New Millenium Women Group, Mama Pinda aliwapongeza wachezaji hao kwa jinsi walivyojituma na kufanikiwa kushinda nafasi ya pili.
 
Alisema vijana hao wamejituma na kufanikiwa kuifunga timu ngumu ya Botswana ambayo kimataifa ina hadhi kubwa kuliko Taifa Queens na kwamba juhudi zao zimeweza kuipandisha hadhi Tanzania katika ulimwengu wa michezo. Aliwatakia ushindi zaidi katika michuano hiyo ambayo mwakani imepangwa kufanyika nchini Malawi.
 
Aliwashukuru Watanzania wote na taasisi ambazo zilijitolea kwa hali na mali kuhakikisha kuwa timu hiyo inafanya vizuri tangu ikiwa kambini hadi wakati wa mashindano.
 
Akitoa shukrani kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha wa timu hiyo, Lilian Sylidion, alisema ahadi ya Mama Tunu Pinda ambayo aliitoa wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Mei 8, mwaka huu iliwapa hamasa na kuchochea kupatikana kwa ushindi huo.
 
“Kwa kweli ile ahadi ya kitita cha shilingi milioni moja ilitufanya tuwe na ari zaidi... kama timu tulidhamiria kuchukua kombe. Mimi binafsi nilisema hata kama ni kuvunjika mguu acha wanivunje lakini nihakikishe siikosi hiyo one m,” alisema huku akishangiliwa na wenzake.
 
Kombe hilo limechukuliwa na Malawi ambao walikuwa ni mabingwa watetezi, Taifa Queens imeibuka washindi wa pili na washindi wa tatu ni Zambia. Malawi wamemaliza mashindano wakiwa na pointi 10 kwa kushinda mechi zote tano wakifuatiwa na Taifa Queens ambayo imepata pointi nane baada ya kushinda mechi nne na kupoteza mechi moja ilipofungwa na Malawi. Zambia imepata pointi sita, Botswana pointi nne, Zimbabwe pointi mbili na Lesotho haikuambulia kitu.
 
Hadi kupata ushindi huo, (Mei 8, 2012) Taifa Queens iliicharaza Lesotho mabao 57 -13, (Mei 9, 2012) Taifa Queens ikafungwa na Malawi 34-30; (Mei 10, 2012) Taifa Queens ikailaza Zambia 37-33; (Mei 11, 2012) Taifa Queens ikaicharaza Zimbabwe 46-15; na jana (Mei 12, 2012) Taifa Queens ikailaza Botswana 32-23.
 
Baadhi ya wake wa viongozi waliohudhuria mechi hiyo pamoja na Mama Tunu Pinda ni Mke wa Makamu wa Rais, Bi. Asha Bilal ambaye alikuwa mgeni rasmi, Mama Hasina Kawawa, Mama Germina Lukuvi, Mama Pamela Matayo, Mama Sophia Mukama, Mama Janet Magufuli, Mama Nahodha, Mama Mwakyembe na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya kuisaidia Taifa Queens ishinde.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA