Waliobomolewa gerezani kulipwa Sh12.3 bilioni

WAKALA wa Usafiri wa Mradi wa Mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam (Dart), umekubali kuwalipa fidia ya Sh12.3 bilioni kwa waliokuwa wakazi wa nyumba zilizokuwa zinamilikiwa na Shirika la Reli Tanzania(TRL) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), eneo la Gerezani Kariakoo,Dar es Salaam.

Uamuzi huo umekuja baada ya wakazi hao kupinga kubomolewa nyumba hizo kupisha mradi wa Dart, jambo ambalo lilisababisha nyumba hizo kubomolewa kwa nguvu Machi 23, mwaka huu.

Akizungumza kwenye mkutano wa pamoja kati ya watendaji wa Dart na wakazi hao, Mkurugenzi Mkuu wa Dart, Cosmas Takule, alisema Serikali imetenga Sh12.3 bilioni kuwalipa fidia wakazi hao.
Takule alisema baada ya kukaa kwa muda mrefu na kujadili, malipo hayo walipaswa kulipwa tangu mwaka 2008, lakini yalichelewa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo baadhi ya wakazi kufungua kesi mahakamani.

“Tulitakiwa kuwalipa tangu mwaka 2008, lakini tulishindwa bada ya baadhi ya wakazi kufungua kesi mahakamani kupinga kubomolewa nyumba hizo, kutokana na hali hiyo tulisubiri hukumu ambayo imemalizika ndiyo tukabomoa,” alisema Takule.

Aliongeza kutokana na vizuizi mbalimbali vilivyojitokeza, Serikali kupitia mradi wa Dart itawalipa fidia hizo na riba kutokana na kuchelewa kwa malipo ya awali.

Takule alisema malipo awamu ya awali ilikuwa Sh11.5 bilioni, kwa wakazi hao na kwamba awamu ya pili watalipa Sh12.3 bilioni ambazo zitaanza kulipwa wakati wowote kuanzia sasa.

“Tunalipa fidia ya ardhi kwa wale waliokuwa wanamiliki viwanja na nyumba, kila mtu aliyebomolewa nyumba yake atalipwa haki yake, hakuna udanganyifu utakaojitokeza katika malipo hayo kutokana na kufanyika kwa usahihi,” alisema. Alisema kutokana na hali hiyo, mradi huo utakamilika mwaka 2014 na kwamba wanaamini mabasi hayo yataanza kazi kipindi hicho.

“Kwa makisio ya awali, mradi utakamilika mwaka 2014 na kutakuwa na mabasi makubwa 150, madogo 220 ambayo yataanza kazi, kutokana na hali hiyo tunaamini kuwa tutatoa ajira kwa watu 180, jambo ambalo litawanufaisha pia Watanzania,” alisema.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Wamiliki wa Nyumba hizo, Rogat Samwel, alisema kitendo cha Serikali kukubali kulipa fidia hizo na riba kitawasaidia kupunguza mahitaji muhimu maeneo watakayokwenda kuishi.

“Tumeridhishwa na malipo hayo, tunachotaka sisi ni utekelezaji siyo ahadi tu, jambo ambalo linaweza kutusaidia kupata fedha hizo kwa ajili ya kutafuta makazi mapya,” alisema Samwel.




Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI