Wapinga uchunguzi kwa watendaji, wadai ripoti ya CAG yatosha

 
WANAHARAKATI nchini wamepinga mpango wa Ikulu wa kutaka kuwapo na uchunguzi wa watendaji katika wizara na taasisi nyingine za umma wanaotuhumiwa kuhusika na ubadhilifu wa fedha za umma kwa kigezo kwamba ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inatosha kuwafikisha mahakamani.

Kauli hiyo imekuja baada ya juzi Ikulu kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuwachunguza watendaji hao na kwamba uchunguzi huo kwa kile walichoeleza ni ili kutomuonea mtu wala kukandamiza wakati wa kuchukua hatua.

Wakichangia maoni katika mada ya hali ya uwajibikaji nchini iliyotolewa kwenye Semina ya Maendeleo na Jinsia (GDSS), iliyofanyika katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) jijini Dar es Salaam walisema , tuhuma zilizowaondoa kwenye nafasi zao ni za kushindwa kuwajibika na si za rushwa.

Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Jinsia katika mtandao huo, Diana Mwiru alisema kwa sasa hakuna haja ya kufanya uchunguzi kwa kuwa ripoti ya CAG na zile za kamati tatu za bunge zinaonyesha wazi namna wahusika walivyohusika katika tuhuma hizo.

“Tuhuma zinazowahusu mawaziri zinatokana na wao kushindwa kuwajibika na kulisababishia hasara taifa, … ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za serikali (CAG) na ripoti za kamati tatu za bunge zote ziko wazi na wote tumeona hasara iliyotokea ,hoja yangu ni kwamba tunachunguza nini tena? alihoji Mwiru na kuongeza:

“Kinachotakiwa kwa sasa ni wahusika kufikisha mahakamani kujibu tuhuma, unafanyika uchunguzi mwingine wa nini, hawa wanatufanya sisi hatujui kitu, kazi ya Takukuru ni kuchunguza rushwa swali ni je tuhuma hizo ni za rushwa? alihoji Mwiru.

Mwiru alisisitiza kuwa chunguzi zilizofanywa zinatosha na sasa watanzania wanataka kuona watuhumiwa wakifikishwa kwenye muhimili mwingine unao tafsiri sheria (Mahakama) ili kuona haki inatendeka.


Mawaziri waliondolewa katika nafasi zao walitajwa katika ripoti ya CAG, na pia ripoti za kamati za kudumu za bunge zilizowasilishwa kwenye vikao vya bunge lilifanyika hivi karibuni mkoani Dodoma.

Kamati hizo ni ile ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (POAC) ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Mwenyekiti wake , James Lembeli zilionyesha namna mawaziri walivyoshindwa kuwajibika na kusababishia taifa hasara kubwa.

Ripoti za kamati hizo Bungeni ziliibua tuhuma za upotevu wa fedha huku zikiwataja baadhi ya mawaziri kushindwa kuwajibika hali iliyomsukuma Bunge wa Kigoma kaskazini, Zitto Kabwe kuitisha hoja ya kukusanya saini za kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Akitoa mada katika washa hiyo, Amina Uddy mwanaharakati toka ForDIA alisema, hali ya uwajibikaji nchini imeshuka kwa kiwango kikubwa hali inayowafanya viongozi washindwe kujali na kusimamia rasilimali za umma.

Alisema ripoti zimebainisha matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma kwenye Mashirika ya Umma, serikali za mitaa na serikali kuu ambapo kuna upotevu mkubwa wa mali za umma ikiwamo suala la ulipaji mishahara hewa.

“Uwajibikaji wa viongozi umepungua, maadili yameporomoka na hii inathibitika wanapotaja mali wakati wa kuingia kwenye nyazifa zao lakini wanapotoka hawataji mali zao, pia hawawajibika katika kulinda rasilimali za nchi” alisema Uddi.

Uddi alitaja sababu zinazochangia hilo kuwa ni pamoja na vitendo vya kuporomoka kwa maadili ya viongozi na mhimili wa Dola kuingilia mamlaka ya utendaji wa mihili mingine ya mahakama na bunge.

“Kitendo cha serikali kufanya uamuzi ni kufanya kazi za bunge, mfano serikali ilitumia Sh544 bilioni bila kuidhinishwa na bunge, Sh1 bilioni zimetumika kulipa mishahara kwa watumishi hewa na Sh3 bilioni zimetumika katika Balozi za Tanzania nje ya nchi zikiwa ni nje ya bajeti iliyoidhinishwa na bunge” alisema Uddi.

Alisema pia uamuzi wa mahakama nao umekuwa ukiingiliwa na dola huku akitoa mfano wa kesi ya mgombea binafsi aliyodai Mahakama kuu imetoa hukumu mara matatu bila mafanikio.

   

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU