WAZEE, VIJANA YANGA WAMBARIKI MANJI

BARAZA la wazee, pamoja na Vijana wa klabu ya Yanga wameunga msimamo uliotolewa na aliyekuwa mfadhili wa zamani wa klabu hiyo, Yusuf Manji kuhusiana na kurejea kwake kuidhamini timu hiyo.
Manji jana aliibuka na kudai kuwa yupo tayari kurudi kuifadhili kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa masharti ikiwemo kuutaka uongozi wa Yanga ukubalike kufanywa uhakiki wa mahesabu ya akaunti za Yanga ndani ya siku 90 na wakaguzi wa hesabu wa kujitegemea kukagua hesabu za kipindi cha 2006 hadi 2012 kwa ajili ya fedha zilizopokelewa na klabu.
Pia kuanzia sasa na kuendelea akaunti za Yanga zichapishwe katika magazeti siku 15 baada ya kumalizika kwa robo ya mwaka, upigaji wa kura ya maoni ndani ya siku 60 na kuamua kama wanachama wa Yanga wanataka kuendesha kampuni ya Yanga au la, ifanye mabadiliko ya katiba ndani ya siku 90 juu ya muundo wake wa uongozi kwa kukubali mojawapo ya mfumo huu chini ya Katiba ya Yanga.
Mwenyekiti wa Vijana wa Yanga, Bakili Makele alisema jana kwamba, masharti aliyoyatoa Manji ni mazuri kwa sababu yatasaidia kuleta uwazi wa baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yamefichwa.
“Tunaunga mkono masharti aliyoyatoa Manji ili kurejea tena kuifadhili Yanga kwani katika hali ya kawaida mtu huwezi kutoa fedha bila kujua zinatumikaje…na ndilo hilo tumekuwa tukilipigia kelele kila siku kwani wanachama tunataka mkutano wa kujua mambo kama haya ili tujiridhishe,”alisema Bakili.
Bakili ambaye aliambatana na wazee wa baraza la Yanga katika kutangaza uwepo wa mkutano wa wanachama kesho makao makuu ya klabu hiyo, alisema kwamba hawana budi kukutana ili kujadili mustakabali wa timu hiyo ambayo kwa sasa ipo katika hali mbaya ya kifedha.
Alisema kutokana na matatizo iliyonayo huenda mali za klabu zikakamatwa na mahakama na hatimaye kupigwa mnada ili kuweza kulipa madeni hayo yanayofikia mil.106 ambapo kesi hiyo ipo Mahakama Kuu.
Makele aliongeza kuwa, leo wanachama wa klabu hiyo toka matawi mbalimbali wanatarajiwa kukutana katika tawi la Buguruni kwa ajili ya kujadili ajenda mbalimbali ambazo watawasilisha katika mkutano huo wa kesho.
Katika hatua nyingine, Katibu wa Baraza la Wazee wa jklabu hiyo Ibrahim Akilimali, amesisitiza viongozi wa kamati ya Utendaji ya Yanga chini ya Mwenyekiti wake Lloyd Nchunga kuondoka madarakani kama walivyowataka awali.
“Tunatoa agizo la mwisho leo (jana) na kesho (leo) kwa Nchunga na wenzake kuachia ngazi, kinyume na hapo watakuwa wamejiwekea sifa mbaya kwani jumapili mvua itawaangukia,”alisema.
Akilimali aliongeza kuwa tayari baadhi ya wanachama wa Yanga kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo Visiwani Zanzibar wameshawasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki katika mkutano huo wa wanachama..Chanzo Dina Ismail Blog

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA